MENEJA WA DIAMOND ATIWA MBARONI KISA DENI LA MILIONI 250
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Tip Top Connection ya jijini Dar es Salaam na Meneja wa
Msanii Diamond Platnumz, Hamis Taletale ‘Babu Tale’, ametiwa mbaroni
na kufikishwa mahakamani na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam
kwa amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Babu
Tale amekamatwa kufuatia amri iliyotolewa Februari 16, 2018 na Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda Maalum, Wilbard Mashauri iliyoelekeza
kukamatwa mtuhumiwa huyo na ndugu yake, Idd Taletale.
Amri
hiyo pia, ilielekeza watakapokamatwa wapelekwe Gereza la Ukonga wakiwa
wafungwa wa kesi ya madai, hadi hapo mahakama hiyo itakapotoa maelekezo
mengine.
Hata
hivyo, Babu Tale hakuweza kupatikana na ndipo mahakama hiyo ikatoa amri
nyingine kama hiyo Aprili 4 mwaka huu. Tangu hapo wamekuwa wakitafutwa
bila mafanikio hadi jana alipokamatwa.
Mahakama
hiyo iliwaamuru kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim
Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya
ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila
ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Baada
ya kutiwa mbaroni leo alifikishwa mahakamani saa tisa alasiri kwa
ajili ya hatua zaidi. Hata hivyo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo,
aliyetoa amri ya kumkamata hakuwepo. Kufuatia kutokuwepo kwa msajili
huyo Taletale amerudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi hadi kesho
asubuhi atakapopelekwa tena mahakamani hapo kwa hatua zaidi.
Hukumu
hiyo iliyomwamuru Babu Tale na nduguye kulipa kiasi hicho cha fedha,
ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa, Februari 18,2016 katika kesi ya
madai namba 185 ya mwaka 2013, iliyofunguliwa na Sheikh Mbonde kutokana
akiwalalamikia ndugu hao kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa
yake.
Comments
Post a Comment