SIMBA WAACHANA NA LECHANTRE KIIVI





Na Mwandishi Wetu, NAKURU
KOCHA Mfaransa wa Simba SC, Pierre Lechantre na Msaidizi wake, Mtunisia Aymen Hbibi Mohammed wameondoka kwenye kambi ya timu nchini kurejea Dar es Salaam kuunganisha usafiri wa kurudi kwao – maana yake kazi basi.
Simba SC inaendeleza ugonjwa wake wa kutodumu na makocha baada ya kutofautiana na Lechantre aliyeanza kazi Januari 18 tu, mwaka huu.
Lechantre na Aymen Hbibi Mohammed jana walikuwa jukwaani wakati Simba SC ikimenyana Simba SC na Kakamega Homeboyz katika Nusu Fainali ya SportPesa Super Cup na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Afraha pia.
Timu iliongozwa na Kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma aliyekaa benchi na kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ na jukwaani alikuwepo Kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’.
Dalili za Simba SC kutodumu na kocha huyo zilianza kuonekana mapema tu baada ya Lechantre kuomba kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon Aprili mwaka huu.
Na baada ya Ligi Kuu kumalizika, Simba SC ikitwaa ubingwa wa kwanza tangu mwaka 2012, iliibuka minong’ono Simba SC haiweze kuendelea na Mfaransa huyo kwa sababu ya mshahara mkubwa.
Lakini pia minong’ono mingine ilikuwa inasema kwamba  viongozi wa Simba hawapendezewi tabia ya ukali wa kupitiliza wa kocha huyo kiasi cha kutopenda hata kuzungumza wala kupokea ushauri.
Na taarifa zilisema asingekuwepo hata kwenye msafara wa timu Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, lakini ikawa toafuti amekwenda ingawa sasa mambo yamekuwa makubwa. 
Haitakuwa ajabu wakati wowote uongozi wa Simba SC ukitangaza rasmi kuachana na Mfaransa huyo ambaye mkataba wake wa miezi sita unafikia tamati mwezi huu.
Lechantre alichukua nafasi ya Mcameroon Joseph Marius Omog na ameiongoza timu katika mechi 22 tu, ukiondoa mchezo wa leo ambao alikuwa jukwaani, ikishinda 14, sare saba na kufungwa moja.
Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Jumapili na mshindi pamoja na kupata dola za Kimarekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England. 
Mshindi wa pili atajipatia dola za Kimarekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500. 
Bingwa mtetezi ni Gor Mahia ambayo mwaka jana iliifunga AFC Leopards 2-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.




Comments

Popular posts from this blog

YANGA YASAFIRI NA HAWA TU , WENGINE WOTE WABAKI NCHINI

YANGA YAJIBIWA HIVI NA TFF KUHUSU KUOMBA KUJITOA KAGAME CUP

MASHINDANO MENGINE TOFAUTI NA KAGAME KUANZA 29, JUNE SIMBA NA YANGA NDANI RATIBA NZIMA HII HAPA