HISTORIA YA KABILA LA WAFIPA KUTOKA SUMBAWANGA





WAFAHAMU WAFIPA..

Wafipa ni jamii ya wabantu waishio katika mkoa wa Rukwa. Shughuli kuu za uchumi kwa jamii hii ni kilimo na ufugaji. Baadhi hujishughulisha na uvuvi na uwindaji.na wale wanaoishi pembeni mwa mto Rukwa hujishughulisha na uvuvi kama moja ya shughuli za kiuchumi. Wafipa wana historia ndefu hasa katika teknolojia ya ufuaji wa chuma kuanzia arne ya 17.
Kama ilivyo kwa jamii nyingi, mila na desturi za wafipa ni suala linaloheshimiwa. Ndoa hufanywa kwa kufuata taratibu za kimila. Kijana akifikia umri wa kuoa hushauriwa na wazazi wake kuhusu ukoo mzuri wa kutafuta mke. Masuala yanayozingatiwa ni pamoja na kuchapa kazi, kuepuka koo zenye magonjwa na zisizokuwa na uzao. Kijana akishaoa hukaa karibu na wazazi kwa muda wa mwaka mmoja ili kujifunza jinsi ya kuendesha familia baada ya hapo huweza kujenga sehemu nyingine.

Wafipa: Kabila lililoamini uwepo wa Mungu wa mbinguni...

WAFIPA ndilo kabila kubwa kuliko mengine yaliyopo katika mkoa wa Rukwa.

Makabila mengine ni Wamambwe, Wanyamangwa na Wakwa ambayo yameishi mkoani humo kwa miaka mingi huku pia ikielezwa kuwa yote haya chimbuko lake ni kabila la Wafipa. Kama ilivyo kwa makabila mengine nchini, Wafipa wana utajiri wa historia ya utamaduni, mila na desturi za kipekee zinazowatofautisha na makabila mengine..

Leo naandika makala haya kuhusu Wafipa, lakini nikajikita zaidi katika utawala wa mwanamke uliopata mafanikio makubwa ambaye pia ndiye mwanzilishi wa jina la Sumbawanga.

Hivi karibuni nilibahatika kutembelea nyumbani kwa mwalimu mstaafu, Angelo January Mbalamwezi (73) na kufanya naye mahojiano ya kina kuhusu mila na tamaduni mbalimbali za kabila hilo ambazo zimekuwa zikipotea taratibu kutokana na mwingiliano wa kijamii na athari za utandawazi.

Mwalimu Mbalamwezi ambaye kwa sasa anaishi eneo la Kizwite, katika Manispaa ya Sumbawanga alistaafu tangu mwaka 1996, wakati huo akifundisha katika Shule ya  Kantalamba.

Alitumia muda wake mwingi kufanya utafiti wa kina wa mila, desturi, uchumi na lugha ya kabila la Wafipa.
Anasema Wafipa ambao kiasili walikuwa wahunzi mahiri wa zana za kilimo pia katika imani ya dini yao ya asili waliamini kwamba kuna Mungu ambaye anaishi juu mbinguni.

Anasema walimtambua Mungu huyu kwa majina kadha wa kadha kama vile Leza kwa maana ya Mungu muumbaji pia walimtambua kama Umwene Nkulu kwamba ni chifu wa machifu wote.

Wafipa pia walimtambua Mungu wa mbinguni kwa jina la Ndaka ambayo maana yake ni jua wakimaanisha kuwa ana nguvu kama jua. Hii inajidhihirisha hata leo ambapo Wafipa wanamtaja Mungu Leza katika salamu zao.

 Kwa mfano wanapokutana wanasalimiana, wanasema Postuta ikimaanisha ; Je, una uzima ndani mwako?
Anayesalimiwa anajibu Tata Itu Kalesa maana yake ikiwa: “Ndio, ninao uzima shauri ya Mungu Baba. Neno “lesa” katika Kalesa ndilo linaloonesha jina Leza ambao kwa sasa Z inatamkika kama S kuonesha jinsi tangu zamani walivyokuwa wakimtukuza Mungu wa Mbinguni.

Pia mtu anaweza kujibu salamu hiyo kwa kusema: Ndakaitu kalesa akimaanisha kuwa niko mzima kwa shauri ya mungu baba ambaye ni jua.

Kumbuka kama tulivyosema hapo juu Ndaka ilimaanisha mungu kama nguvu ya jua.

 Wafipa waliamini kuwa mungu wao waliyemtambua kama Lesa anaishi huko mbinguni na kwamba alimuumba binadamu wa kwanza aitwaye Ntatakwa na akamteremsha katika Mlima Itwelele uliopo hadi sasa katika kijiji cha Milanzi katika Manispaa ya Sumbawanga.

Wanasema binadamu huyo wa kwanza alivimba mguu na ulipopasuka akatokea mkewe aitwaye Kao. Wanaamini pia kuwa Mlima Itwelele na hususan pango lililo katika mlima huo ni sehemu takatifu ambapo walikuwa wakiabudu na kutoa sadaka zao kwa mungu wao.

Kwa imani ya dini hiyo ya asili ya Wafipa Leza (lesa) aliumba miungu wengine wadogo ambao walikuwa wasaidizi wake kwani ilikuwa rahisi kwa Wafipa kuwafikia miungu hao wadogo kirahisi na kuwa kiungo muhimu kati yao na Leza aliye mbinguni. Na kwa imani yao miungu hao wadogo waliishi katika vyanzo vya maji na katika misitu au milimani, kwa mfano wanaamini kwamba katika Mlima Itwelele aliishi mmoja wa miungu wadogo wa kiume ambapo mkewe aliishi katika Mlima Kalangasa, jirani na hapo.

Pia kulikuwa na mmoja wa miungu wadogo wa kike akitwaye Katai aliyeishi katika kichuguu kilipojengwa sasa kiwanda cha unga, eneo la Kizwite, katika Manispaa ya Sumbawanga. “Mungu huyu mdogo wa kike ambaye Wafipa walimwita Katai kule Mpanda wao walimwita Katavi, lakini alikuwa ni mungu wa kiume… Sasa basi Wafipa waliweza kuwaendea miungu hawa wadogo kwa kufanya matambiko wakati wanapokumbwa na majanga au magonjwa na kuwatolea sadaka,” anasema Mzee Mbalamwezi.

Kadhalika anasema kuwa viongozi wa kiroho walikuwa watemi ama wakiitwa mwene. Katika Mlima Itwelele kwa mfano, kuna pango hivyo kupitia mwene (mtemi) walitoa sadaka ambazo mara nyingi ilikuwa mbuzi mweupe. Rangi nyeupe ilichukuliwa kuwa ni alama ya usafi.

Hivyo mwene akisaidiwa na mzee maarufu aliyejulikana kama kapepa, Wafipa walitoa sadaka hizo kwa kuzichoma karibu na pango lililopo katika Mlima Itwelele na moshi ukielekea juu mbinguni ilikuwa ni dalili ya kuwa lesa ameikubali sadaka hiyo. Baada ya kutolewa na kupokelewa kwa sadaka hiyo nyama ya mbuzi huyo ilikatwa katwa vipande na kupewa watu maarufu kijijini ikiwa ni ishara ya kuwa wameshiriki kikamilifu katika kumtolea lesa sadaka hiyo takatifu.

Hivyo kama kulikuwa na ukame na magonjwa baada ya kupokelewa kwa sadaka hiyo na lesa, mvua ilianza kunyesha na kero ya magonjwa ilitoweka na watu waliendelea kuwa na siha njema. Katika imani hiyo vijana walifundishwa kuwathamini na kuwaheshimu watu waliowazidi umri.
Utii kwa wakubwa ulisisitizwa sana kwa kuwa Mfipa alijengwa kuamini pia kwamba watu wakubwa kwa umri ni wawakilishi wa Lesa hapa duniani. Ilikuwa marufuku kwa mtu yeyote kufanya uharibifu katika vyanzo vya maji na misitu wakiamini kuwa ni chanzo cha uhai pia yalikuwa makazi ya miungu wao, hivyo ilikuwa ni marufuku kuvichezea ovyo.

Pia walikuwa na sherehe kubwa mbili kwa mwaka, kabla ya kunyesha kwa mvua na baada ya mavuno ambapo walitoa sadaka ya mazao na pombe kwa lesa ikiwa ni dalili ya kumtolea heshima na kumshukuru kwa neema ya mvua na mavuno mazuri aliyowajalia.
“Hata wazee wengine wakati wa mavuno walikoroga pombe majumbani mwao kisha kiasi wakaiweka kwenye kibuyu kando ya nyumba zao ili mungu wao nae aonje kazi ya mikono ya waja wake,” anaeleza Mzee Mbalamwezi. Chakula kikuu cha Wafipa kinaelezwa kuwa ni ugali wa ulezi na maharage na mwanamke hakuruhusiwa kula mayai wala nyama ya kuku.
Waliamini kuwa iwapo kama mwanamke angekula nyama ya kuku na mayai wakati wa kujifungua angepata matatizo makubwa kwa kuwa mtoto wakati wa ujauzito wake angekuwa mnene sana. Lakini mwanamke baada ya kujifungua, licha ya kulishwa vyakula vya aina mbalimbali ili kuhakikisha siha yake inaimarika haraka, pia aliruhusiwa kwa wakati huo kunywa mchuzi wa kuku.
Anapochinjwa kuku, filigisi iliandaliwa rasmi kwa ajili ya baba mwenye nyumba kwa mgeni aliyesababisha kuku kuchinjwa na si vinginevyo. Kadhalika masimulizi ya Mzee Mbalamwezi yanaonesha kwamba pombe iliyotengenezwa kwa ulezi maarufu ‘kimpumu’ ni kinywaji kilichothaminiwa sana na kupendwa.
Anasema pombe hiyo ilikuwa ikinywewa kwa mirija na watu wa rika zote wakiwemo watoto wakati wa jioni na hasa baada ya shughuli za kilimo. Pombe hiyo pia ilitumika katika sherehe za harusi na misiba. Kadhalika Wafipa waliamini kuwa kulikuwa na maisha baada ya kifo ambapo mtu mwema ‘mtakatifu’ alizaliwa tena upya katika familia aliyotoka na mtu mbaya akijulikana kama ‘chiswa’, aliogopeka sana katika jamii.

Wafipa waliamini kwamba baada ya kufa mtu mbaya alirejea na kuwasumbua kama mzimu mbaya. “Mfano, mimi nilipozaliwa wazazi wangu walinitazama kisha wakaamua kuniita Kalimina likiwa ni jina la babu yangu aliyekufa kitambo wakiamini kuwa nimezaliwa nikifanana naye na hivyo babu amerudi tena katika familia yetu kupitia mimi,” anasema Mzee Mbalamwezi.

Anasema Wafipa waliamini kuwa dhambi kubwa kuliko zote ni kuua mtu kwani kwao mtu yeyote ni mali ya mungu wao lesa, hivyo kulikuwa hakuna mwenye mamlaka duniani ya kutoa uhai wa mtu isipokuwa lesa pekee.

Kuhusu mavazi ya Wafipa ya Asili, Mzee Mbalamwezi anasimulia kwamba wanaume wa Kifipa walikuwa wakivaa kipande cha ngozi ya ng’ombe au mbuzi kwa ajili ya kujisitiri sehemu za siri tu huku mwili mwingine ukibaki wazi.

Kwa upande wa wanawake anasema walivaa vipande vya ngozi za wanyama kujisitiri sehemu zao za siri na kufunika matiti. Kadhalika walivaa shanga kiunoni na shingoni.
Anasema baadaye Wafipa walianza kuvaa vipande vya nguo, hususan kaniki ambazo zilikuwa zikitengenezwa na jirani zao wa kabila la Wakwa waishio katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga kwa sasa.

Inaelezwa kuwa Wakwe enzi hizo walikuwa wakulima hodari wa pamba ambapo baadaye walivumbua kinu cha kuchambua nyuzi za pamba kisha wakaanzisha ‘kiwanda’ cha kutengeneza nguo za pamba.

Mila na desturi hizi za Wafipa ikiwemo lugha yao vimeanza kutoweka kwa kasi kutokana na kile kinachoelezwa vijana kujikuta wamegubikwa na kuhadaika na utandawazi na kuanza kuiga mila na desturi za watu wengine.

Ni vyema sasa historia na tafiti kama Mzee Mbalamwezi ambazo hazijawekwa kwenye vitabu zikaungwa mkono ili ziweze kuhifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho...

Comments

Popular posts from this blog

YANGA YASAFIRI NA HAWA TU , WENGINE WOTE WABAKI NCHINI

YANGA YAJIBIWA HIVI NA TFF KUHUSU KUOMBA KUJITOA KAGAME CUP

MASHINDANO MENGINE TOFAUTI NA KAGAME KUANZA 29, JUNE SIMBA NA YANGA NDANI RATIBA NZIMA HII HAPA